Hotline: (+255) 24-2230271 Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

 

Sub Page Name

×

Warning

JUser: :_load: Unable to load user with ID: 305

Wakuu wa Mikoa Wahimiza Uimarishaji Zao la Karafuu, Kuimarisha Uchumi

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idrisa Muslim Hija amelishauri Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuangalia uwezekano wa kuanzisha taasisi maalum itakayoshughulikia tafiti za kitaalamu juu ya zao la karafuu.

Alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la karafuu katika mkutano maalum ulioandaliwa na Shirika la ZSTC kwa Wakulima na wadau wa zao hilo Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kutokana na zao la karafuu kuendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na wananchi wake ambapo wananchi wengi wanaonyesha nia na ari ya kulima zao hilo hivyo wanahitaji msaada mkubwa wa kitaalamu juu ya ukulima wa zao hilo.

Alisema endapo itaanzishwa taasisi hiyo ya utafiti itatoa majibu ya changamoto zinazokabili zao hilo mashambani ikiwemo udongo unaokubali kuota mikarafuu, njia bora za upandaji, mbegu bora, maradhi na tiba yake.

Alisema pamoja na kuwepo kwa Wizara ya kilimo na Shirika la ZSTC ambazo zinatoa huduma za uimarishaji wa zao hilo la karafuu lakini taasisi hizo zina majukumu mengine zaidi  hivyo itakuwa ni busara endapo itaanzishwa taasisi maalum itakayohusika moja kwa moja kufanya utafiti na kuja na majibu ya kitaalamu.

Akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la karafuu wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa huo Bi. Mwanajuma Majid Abdalla, aliwakumbusha Wakulima wa zao hilo la karafuu kuendelea kulinda ubora, kuacha kabisa magendo na kuuza karafuu zote Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC.

Alisema Sheria ya Maendeleo ya Karafuu Na. 2 ya mwaka 2014 ipo kwa ajili ya kulinda zao la karafuu kwa maslahi ya nchi na wananchi wake ambapo aliwataka Masheha kuwafahamu wakulima wa zao la karafuu katika shehia zao ili kuimarisha ulinzi.

Aliwataka Masheha kuhakikisha karafuu hazihamishwi kutoka sehemu moja kwenda nyengine kinyume na utaratibu uliowekwa wa kuomba kibali ambapo  alifahamisha kuwa uhamishaji kiholela unaweza kupelekea watu waovu kutumia nafasi hiyo kusafirisha magendo.

Aidha Bi. Mwanajuma aliwasisitiza Wakulima na Wadau wa zao la karafuu kujisajili haraka kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Shirika la ZSTC ili kunufaika na huduma za uendelezaji wa zao la karafuu.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein anaonyesha imani kubwa na wakulima wa zao la karafuu hivyo huduma kwa wakulima hao zitaendelea kutolewa hivyo ni vyema wakulima wote na wadau wa zao la karafuu wakajisajili ili wafahamike rasmi na kupatiwa huduma.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman alisema hataki kuona mkoa wake ukichafuliwa kwa biashara za magendo ya karafuu wala kuwepo kwa viwanda vya kuchafua karafuu kwa makusudi.

Akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la karafuu kwa nyakati tofauti, alisema Mkoa huo wa Kaskazini unazungumzwa sana kwa magendo ya karafuu kutokana na bahari yake kupakana na nchi za jirani hivyo inawezekana waovu wanatumia kama njia ya kutoroshea karafuu, alisema hatokubali vitendo hivyo viendelee kutokea katika Mkoa wake.

Aliwataka Wakulima katika Mkoa huo kufuata maagizo wanayopewa na wataalamu juu ya kulinda ubora wa zao la karafuu na kuacha kabisa kuanika karafuu barabarani, juu ya mabati, sakafuni na kuchafua kwa makusudi.

Akiwasilisha tathmini ya manunuzi ya karafuu mwaka 2016/2017 katika mikutano hiyo Mkurugenzi Fedha wa Shirika la ZSTC Imail Omar Bai alisema katika mwaka huo wa 2016/2017 hadi kufika tarehe 30/04/2017 Shirika limenunua karafuu kutoka kwa Wakulima jumla ya tani 2,266.2 zenye thamani ya TZS 31.8 bilioni Unguja na Pemba.

Alifafanua kuwa Unguja zimenunuliwa tani 132.5 kwa thamani ya TZS 1.8 bilioni na Pemba zimenunuliwa tani 2,133.7 kwa thamani ya 29.9 bilioni. Manunuzi hayo  ni sawa na asilimia  81 ya makadirio  yaliyowekwa na Shirika la ZSTC kwa mwaka wa 2016/2017.

Alifahamisha kuwa makadirio kwa mwaka wa 2016/2017 ilikuwa ni kununua tani 2,810, Unguja tani 160.0 na Pemba 2,650.0 ambapo aliwapongeza na kuwashukuru Wakulima na Wafanyabiashara ya karafuu kwa kuuza karafuu zao Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC.

Kwa upande wao Wakulima na Wadau wa zao la karafuu waliendela kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa namna wanavyoshirikiana na Wakulima katika kulihudumia zao la karafuu.

Pamoja na pongezi hizo Wakulima hao waliendelea  kuiomba Serikali kuwa karibu na kuzidisha huduma zaidi kwa Wakulima wa zao hilo la sekta ya karafuu kwa jumla kwa vile uimarishaji wa zao hilo ni kazi ngumu.

Walifahamisha kuwa kumekuwa na kipindi kirefu cha jua na joto limeongezeka kunakosababisha uotaji na ukuaji wa mikarafuu kuwa mgumu hivyo kuhitaji jitihada zaidi za wakulima. Waliomba Serikali kuangalia uwezekano wa kusaidia huduma za maji katika mashamba ya mikarafuu ikiwemo kuwachimbia visima.

Wakibainisha changomoto nyengine kubwa katika ukulima wa zao hilo la karafuu wakulima hao walisema kuwa wafugaji wamekuwa tatizo kubwa kwao kutokana na tabia zao za kuingiza mifugo yao katika mashamba ya mikarafuu na kuathiri zao hilo.

 

Rate this item
(2 votes)

Contact Us
Why ZSTC?

We offer the best quality of Cloves in the market that has a strong taste and aroma. We offer the best price and it is negotiable.  Considering our terms of sales we do on-time shipment of your purchases. We provide free samples while attempting to try and purchase.

We're Open :0730 -1630Hrs EAT Mon-Friday
Sunday and Public Holidays: Closed